KVDA YALENGA KUIMARISHA UZALISHAJI WA ASALI KERIO VALLEY.


Mamlaka ya ustawishaji wa maendeleo kwenye bonde la kerio KVDA inashirikiana na idara ya mifugo katika wizara ya kilimo kuimarisha uzalishaji wa asali humu nchini.
Kwa mujibu wa meneja mkurugenzi wa KVDA Sammy Naporos taifa hili bado lina upungufu mkubwa wa asali na huagiza takriban asilimia hamsini ya bidhaa hiyo muhimu inayotumika humu nchini.
Amesema kwamba mpango huo unalenga takriban kaunti sita kwenye eneo la kaskazini mwa bonde la ufa ili kuhakikisha kwamba asali ambayo inazalishwa humu nchini inatosheleza mahitaji na kuuzwa kwenye mataifa ya kigeni.
Aidha mamlaka hiyo imetenga kima cha shilingi milioni sitini za kununua asali kutoka kwa vyama vya ushirika vya wakulima hasa kwenye kaunti hii ya Pokot magharibi na Baringo.
Amedokeza kwamba asali inayozalishwa katika kaunti ya Pokot magharibi ni miongoni mwa asali bora zaidi duniani na imewasaidia wakaazi kupata mapato ya kuridhisha.
Hata hivyo, Naporos amesema kwamba mizinga ambayo inatumika na wazilishaji ni za asili hali ambayo inaathiri pakubwa kiwango cha asali kinachozalishwa.