‘KUTUPILIWA MBALI BBI KUNAFAA KUWA FUNZO KWA VIONGOZI WA POKOT MAGHARIBI.’ MOROTO.

Hisia mseto zimeendelea kuibuliwa miongoni mwa viongozi kufuatia hatua ya mahakama ya rufaa kudumisha uamuzi wa mahakama kuu wa kutupilia mbali mchakato wa kufanyia katiba marekebisho kupitia mpango wa BBI.
Mbunge wa kapenguria katika kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Moroto amepongeza uamuzi huo wa mahakama akisema kuwa umemwegemea zaidi mwananchi wa kawaida kwani mchakato mzima wa BBI haukuwahusisha wananchi bali ulikuwa mradi wa watu wachache waliotaka kujinufaisha kibinafsi.
Moroto amesema kuwa uamuzi huo wa mahakama unastahili kuwa funzo kwa viongozi wa kaunti hii ya pokot magharibi kufanya kazi kwa ushirikiano na umoja kwa manufaa ya mkazi wa kaunti hii na kutokuwa na ubinafsi.
Wakati uo huo Moroto amepuuzilia mbali madai kuwa huenda baadhi ya maswala ambayo yalikuwa yakishinikizwa kupitia mchakato wa BBI ikiwemo kubuniwa maeneo bunge mapya yakazimwa kufuatia uamuzi huo wa mahakama akisema swala la kubuniwa maeneo bunge mapya lilikuwepo hata kabla ya ujio wa BBI.