KUPPET YAIONYA TSC KUHUSU SHULE ZA UPILI ZISIZO NA WALIMU WAKUU POKOT MAGHARIBI.

 Na Benson Aswani.

Tume ya huduma kwa walimu nchini TSC imetakiwa kuharakisha mchakato wa kuwatuma walimu wakuu katika shule za upili ambazo hazina wakuu hao katika kaunti ya Pokot magharibi.

Akizungumza afisini mwake katibu mkuu wa chama cha walimu wa shule za upili na vyuo vya kadri KUPPET tawi la kaunti ya Pokot magharibi Alfred Kamuto, alisema kwamba zipo takriban shule 20 katika kaunti hiyo ambazo hazina walimu wakuu.

Kamuto alitoa wito kwa mkurugenzi wa tume hiyo kanda ya bonde la ufa kuhakikisha kwamba swala hilo linashughulikiwa haraka iwezekanavyo, kwani ukosefu wa wakuu hao unatatiza shughuli za masomo katika shule hizo kutokana na majukumu muhimu ambayo yanahitaji uwepo wa walimu hao.

Kuna takriban shule 20 ambazo hazina walimu wakuu. Ningependa kuhimiza tume ya huduma kwa walimu TSC waharakishe mchakato wa kuwatuma walimu wakuu katika shule hizi, ili masomo yaendelee kwa sababu ilivyo sasa shughuli za masomo zimeathirika katika shule hizo.” Alisema Kamuto.

Aidha Kamuto alisema kwamba huenda chama hicho cha KUPPET kwa ushirikiano na kile cha KNUT vikaongoza maandamano ya wazazi hadi afisi za tume hiyo kushinikiza kuondolewa afisini mkurugenzi wake kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake na kulemaza shughuli katika shule husika.

“Iwapo tume hiyo haitafanya hivyo, basi sisi kama wawakilishi wa walimu pamoja na chama cha KNUT tutaandaa maandamano ya wazazi hadi afisi ya mkurugenzi wa tume hiyo kanda hii na hata kushinikiza kuondolewa afisini kwa sababu ni kama yeye ndiye tatizo.” Alisema Kamuto.