KUPIGWA MARUFUKU POMBE KWAIMARISHA HALI YA MAISHA KABICHBICH


Maisha ya wakazi wa eneo la Kabichbich, Lelan kaunti hii ya Pokot magharibi yameimarika pakubwa tangu kupigwa marufuku ugemaji pombe haramu na pia uuzaji aina yoyote ya pombe eneo hilo hali iliyochochewa pakubwa na wazee.
Wakiongozwa na Jackson Mnangat, wazee hao wamesema kuwa msingi uliowekwa na chifu wa kwanza wa eneo hilo baada ya wazee kuongoza kampeni hiyo iliyopelekea kupigwa kura na kuungwa mkono na idadi kubwa ya wenyeji, umepelekea wakazi wengi kujihusisha na shughuli muhimu ambazo zimeimarisha maisha yao.
Aidha baadhi ya wakuu wa shule wakiongozwa na mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya St Kizito Kabichbich Thomus Ombati wamesema hatua hiyo imepelekea kuimarika viwango vya elimu kwani wazazi wengi wamekumbatia elimu kwa kuwapeleka wanao shuleni, baadhi ya shule zikirekodi kuimarika matokeo katika mitihani ya kitaifa.
Chifu wa eneo hilo Daniel Nguriatudo amethibitisha hali hiyo akisema kuwa wataendelea kushikilia hilo ili kuhakikisha maisha ya wakazi yanaendelea kuimarika.