KUP CHAIKARANGA UDA POKOT KUSINI NA KACHELIBA.


Hatimaye David Pkosing amehifadhi kiti chake katika Eneo bunge la Pokot Kusini kaunti hii ya Pokot magharibi baada ya kumpiku mpinzani wake wa Chama Cha UDA Simon Kalekem kwa kura elfu 13,029.
Pkosing aliibuka mshindi katika Eneobunge hilo baada ya kuzoa kura elfu 28,250 kupitia kwa Chama Cha KUP.
Simon Kalekem wa UDA alipata kura elfu 15,221huku James Teko ambaye amekuwa mgombea huru akizoa kura elfu 2,549.
Akizungumza kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayo, teko alikubali kushindwa huku akiahidi kushirikiana na mshindi David Pkosing.
“Kinyang’anyiro kimekuwa kizuri na ilivyo sheria za kinyang’anyiro chochote, pana mshindi na mshinde, nachukua fursa hii kukubali kushindwa na kuahidi kushirikiana na atakayetangazwa mshindi kwa manufaa ya wakazi wa eneo hili.” Alisema.
Wakati uo huo Titus Lotee ndiye ameibuka bora katika Eneo bunge la Kacheliba kupitia kwa Chama Cha KUP na kumpiku Mark Lomunokol wa UDA.
Lotee alizoa kura elfu 20,073 dhidi ya elfu 17,963 za mpinza wake wa UDA mbunge wa sasa Mark Lomunokol huku John Lodinyo akipata kura elfu 1,346.
Ni ushindi ambao ulipongezwa na wakazi wa eneo hilo wakielezea imani kwamba Lotee ataimarisha maisha yao kutokana na kile wamedai wamepitia mahangaiko makubwa chini ya mbunge anayeondoka Mark Lumnokol, wakitaja uhaba wa maji na na kutelekezwa sekta ya afya kama moja ya matatizo yanayowakabili.
“Nimefurahi sana kwa ushindi wa Lotee Titus, tumempigia kura ili aje aimarishe maisha yetu kwa sababu hatuna maji, hatuna dawa kwa hospitali, barabara ni mbovu. Kwa hivyo tuna uhakika kwamba Lotee atatusaidia.” Walisema.