KUONDOLEWA MARUFUKU YA KUTOKUWA NJE USIKU KWAENDELEA KUPONGEZWA.

Na Benson Aswani
Hatua ya rais Uhuru Kenyatta kuondoa amri ya kutokuwa nje kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri ili kukabili msambao wa virusi vya corona imepokelewa vyema na wakenya wa matabaka mbali mbali.
Wa hivi punde kupongeza uamuzi huo ni mwakilishi wadi wa Lelan kaunti hii ya Pokot magharibi Johnson Lokato ambaye amesema kuwa amri hiyo ililemaza shughuli nyingi nchini ikiwemo biashara na hata wakazi wengi kupoteza maisha yao kwa kukosa mbinu za kufika hospitalini.
Aidha Lokato amesema kuwa hatua hiyo italeta afueni hasa kwa maafisa wa usalama ambao walitumia muda mwingi kwenye kijibaridi kutekeleza majukumu ya kuhakikisha kuwa hamna mkenya ambaye anavunja amri hiyo.
Wakati uo huo Lokato amependekeza kufanya lazima kwa kila mtu mwenye umri wa miaka 40 na zaidi kupata chanjo dhidi ya virusi vya corona, pamoja na kuwekwa mikakati ya kuhakikisha wakenya wengi wanachanjwa ili kuwe na usalama wa kutosha nchini dhidi ya janga hili.