KUNDI MOJA LAONGOZA MATEMBEZI YA KILOMITA 367 KUHIMIZA AMANI KASKAZINI MWA BONDE LA UFA.

Kundi moja linaloshughulikia maswala ya amani kutoka kaunti Jirani ya Turkana limeungana na viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi katika matembezi ya kuhimiza amani miongoni mwa jamii za Turkana na Pokot.

Akizungumza na wanahabari baada ya kuongoza matembezi hayo kwa kilomita 257 ambapo wanalenga kutembea kilomita 367 hadi mjini Eldoret, balozi wa amani kaunti ya Turkana ambaye ndiye kiongozi wa kundi hilo Dkt Chales Lochodo alisema kwamba amani itapatikana tu maeneo haya kupitia kujitokeza kwa viongozi kuhimiza hilo.

“Amani haipatikani afisini. Amani itapatikana tu iwapo viongozi wote tutajitokeza na kwenda mashinani kuwaongelesha vijana kujitenga na visa vya uhalifu. Tuwache kuwafadhili ndugu zetu kuendeleza uovu huu.” Alisema Lochodo.

Ni ujumbe ambao ulisisitizwa na mkewe mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto, Mary Moroto ambaye alisema kwamba ni kina mama na watoto ndio huhangaika pakubwa kunaposhuhudiwa uvamizi huu.

“Kunapokuwa na vita ni mama na mtoto ndio huhangaika. Nilisikia huu wito na kusema daktari hataenda peke yake. Tutashikana naye na tunajua kwamba Mungu ataokoa nchi yetu.” Alisema Bi. Mary Moroto.

Viongozi wengine katika kaunti hiyo walioshiriki matembezi hayo wakiongozwa na waziri wa utamaduni michezo na maswala ya vijana Joshua Siwanyang, walilitaka kundi hilo kuelekeza ujumbe wake hasa maeneo ambayo yanakumbwa na tatizo la utovu wa usalama ili kuwahamasisha wakazi wa maeneo hayo kuhusu umuhimu wa kuishi kwa umoja.

“Ninachohimiza kundi hili ni kwamba waelekeza ujumbe huu zaidi maeneo ambako kumekuwa kukishuhudiwa uvamizi wa mara kwa mara ili watu wa maeneo haya wahimizwe umuhi mu wa kuishi kwa amani.” Alisema Siwanyang.