KUKITHIRI MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA NA POMBE KWAIBUA HOFU KACHELIBA.

Wakazi wa Kacheliba katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kulalamikia kukithiri matumizi ya mihadarati na pombe miongoni mwa vijana.

Wakiongozwa na kiongozi wa vijana eneo hilo Job Wanjala wakazi hao walisema wengi wa vijana wamezama katika matumizi ya mihadarati na pombe hali ambayo imechangia kukithiri utovu wa usalama eneo hilo kutokana na hatua ya baadhi kubomoa maduka na kupora mali ya wakazi.

“Vijana wengi wamezama kwenye matumizi ya pombe na bangi. Miaka ijayo sidhani kama tutakuwa na vijana kwa sababu sasa wote hawajitambui, kazi ni kuvuta bangi na kunywa pombe. Hata sasa huku usalama umeharibika kwa sababu wanabomoa maduka na kuiba mali ya watu.” Alisema wanjala.

Aidha baadhi ya wazazi wamelalamikia kupotoka pakubwa maadili miongoni mwa vijana hao wakitoa wito kwa idara ya usalama eneo hilo kuingilia kati na kukabili visa hivyo kabla ya hali kuwa mbaya zaidi.

“Tunaomba serikiali iingilie kati na kuokoa hawa vijana na kama kuna yule atapatikana na bangi anapasa kukamatwa na kuchukuliwa hatua, kwa sababu sasa wengi wao hata hawana nidhamu kwa wazazi wao.” Walisema.

Akikiri kukithiri visa hivyo OCS wa kituo cha polisi cha Kacheliba Tom Nyanaro alisema kwamba wapo baadhi ya wahusika ambao wametiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani kwa kujihusisha na tabia hiyo na kwa sasa wanaendeleza uhamasisho kwa vijana kuhusu athari za matumizi ya pombe na mihadarati.

“Mwezi jana tuliwakamata watu wawili na kuwafikisha mahakanani kwa kupatikana wakiendeleza biashara ya kuuza bangi. Lakini kwa sasa tunaendeleza uhamasisho kwa vijana kuhusu athari za matumizi ya bangi na pombe.” Alisema Nyanaro.