KUFUNGULIWA KANISA LA ELCK DAYOSISI YA KERIO VALLEY KWATAJWA KUWA HATUA KUFIKIA SULUHU KWA UTOVU WA USALAMA MAENEO YA MIPAKANI.
Na Benson Aswani.
Swala la utovu wa usalama katika bonde la kerio lilitawala hafla ya kutawazwa rasmi kwa askofu mpya wa kanisa la ELCK dayosisi ya kerio valley ambayo iliandaliwa eneo la Chester eneo bunge la Sigor katika kaunti ya Pokot magharibi.
Wakizungumza katika hafla hiyo viongozi kaunti hiyo walisifia kubuniwa kwa dayosisi hiyo ambayo walisema itasaidia pakubwa kwa viongozi wa kidini kueneza injili maeneo ambako ilikuwa vigumu kwa viongozi wa kidini kufika hasa sehemu ambazo zimeathirika pakubwa na utovu wa usalama.
“Kubuniwa kwa dayosisi hii ni muhimu sana ikizingatiwa maeneo haya yamekuwa yakishuhudia utovu wa usalama kwa miaka mingi. Dayosisi hii sasa itawawezesha viongozi wa kidini kuingia katika maeneo haya na kueneza injili ambayo itapelekea kukabili uhalifu.” Walisema viongozi.
Ni kauli ambayo ilisisitizwa na uongozi wa kanisa hilo ambao pia ulitoa wito kwa serikali kuhakikisha kwamba shule ambazo bado hazijafunguliwa maeneo yaliyoathirika na utovu wa usalama zinafunguliwa, wakielezea imani kwamba amani itapatikana kupitia harakati za kanisa hilo.
“Tunaomba serikali kufungua shule ambazo bado hazijafunguliwa maeneo haya kwa sababu sisi tuna imani kwamba ujio wa kanisa hili utasaidia kukabili visa vya utovu wa usalama.” Walisema.
Naye mkurugenzi wa mipango katika afisi ya mkewe naibu rais ambaye alikuwa mgeni wa heshima katika hafla hiyo askofu Wilson Kosgei, alisema kutelekezwa mtoto wa kiume ndiko kumesababisha wengine wao kujihusisha na uhalifu akitaka hali hiyo kushughulikiwa.
“Kwa miaka mingi tumekuwa tukitilia mkazo maswala ya mtoto wa kike na kumsahau mtoto wa kiume. Hali hii imesababisha wengi wao kuanza kujihusisha na visa vya uhalifu kwa kuona kuwa jamii imewatenga. Tunapasa kushughulikia hali hii kwa dharura.” Alisema Kosgei.
Kwa upande wake askofu wa kanisa hilo la ELCK Thomas Lokori, alitoa wito kwa serikali pamoja na viongozi wa kisiasa, kushirikiana nao katika kuhakikisha amani inadumishwa maeneo haya kupitia kwa ujenzi wa shule na hospitali, alizosema kwamba zitakuwa za msaada katika juhudi za kuafikiwa amani.
“Tunaomba serikali pamoja na viongozi wa kisiasa kushirikiana nasi kwa ukamilifu kwa kuhakikisha kwamba wanajenga shule zaidi pamoja na hospitali wakati sisi tutakuwa tukieneza neon la Mungu ili tuhakikishe kwamba usalama unaafikiwa kwa ukamilifu.” Alisema Lokori.