KOMONGIRO ATETEA BARAZA LA MAWAZIRI POKOT MAGHARIBI.
Mwakilishi wadi ya Sook katika kaunti hii ya Pokot magharibi Martine Komongiro ametetea uteuzi wa maafisa wanaohudumu katika serikali ya gavana Simon Kachapin kufuatia lalama za baadhi kuwa waliahidiwa nafasi ila hawakuteuliwa.
Komongiro ambaye pia ni kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti hii ya Pokot magharibi alisema kwamba gavana Kachapin hafai kulaumiwa kwani hajafanya kosa lolote katika uteuzi wa baraza lake la mawaziri akisisitiza kwamba nafasi serikalini ni chache ikilinganishwa na wanaohitaji.
“Hamna mtu wa kulaumiwa hapa kwa sasa nafasi za kazi ni chache na wanaohitaji ni wengi. Kwa hivyo gavana hajafanya kosa lolote hadi kufikia sasa katika uteuzi wa baraza lake la mawaziri.” Alisema Komongiro.
Komongiro aliwahimiza wote waliotarajia kuteuliwa katika baraza hilo ila wakakosa nafasi kutokufa moyo kwani gavana Kachapin hajakamilisha kubuni serikali yake ikizingatiwa bado makatibu wa wizara mbali mbali na wakurugenzi hawajateuliwa.
“Nataka kuwatia moyo wale ambao labda waliahidiwa nafasi katika serikali ya gavana Kachapin, au labda waliona kuwa walistahili kupewa nafasi hizo na wakakosa kuwa wasikate tamaa. Kuna nafasi ambazo bado hazijajazwa kama vile makatibu na wakurugenzi.” Alisema.