KOMOLE AKANA RIPOTI KUWA POKOT MAGHARIBI HAIJAATHIRIKA NA BAA LA NJAA.

Naibu gavana kaunti hii ya Pokot magharibi Robert Komole amepinga vikali ripoti inayoonyesha kwamba kaunti hii haijaathirika pakubwa na baa la njaa ilivyo katika kaunti 23 ambazo zimetajwa kukumbwa na makali hayo.

Akizungumza baada ya kikao cha kuangazia athari za baa la njaa na wadau mbali mbali Komole alisema kuwa wakazi katika maeneo mengi ya kaunti hii wanakabiliwa na baa la njaa akiwataka wanaotoa ripoti kuhusu kaunti athirika kutoa ripoti kamili kuhusu hali katika kaunti hii ili wakazi waweze pia kunufaika na msaada unaotolewa na serikali kuu.

“Ripoti ambazo tumepata ni kuwa watu wa pokot magharibi ambao wameathirika na baa la njaa ni wachache, na tunapinga ripoti hiyo kwa sababu watu wengi maeneo ya pokot ya kati, eneo bunge la sigor na huko Chepkono wameathirika na baa la njaa na tunaomba wanaotoa ripoti hizi watoe ripoti za kweli ili wakazi wa kaunti hii pia wanufaike kama kaunti zingine.” Alisema Komole.

Aidha Komole alisema serikali ya kaunti inaweka mikakati ya kuhakikisha kwamba wakazi wa kaunti hii ambao wameathirika na baa la njaa wanasaidika ikiwemo kutenga kiasi fulani cha fedha katika bajeti ya kwanza ya ziada.

“Tunajaribu kuangalia bajeti ya ziada tuone kama tunaweza kuweka pesa kidogo za kusaidia wakazi wetu wa Pokot magharibi ili waweze kupata chakula.” Alisema.

Kwa upande wake afisa katika idara ya kukabili majanga NDMA Joshua Mayeku alisema kwamba wahisani zaidi wamejitokeza kusaidia katika kusambaza msaada kwa waathiriwa na kwa sasa wanaendeleza ukaguzi wa maeneo ambayo yatapewa kipau mbele katika shughuli hiyo.

“Washirika mbali mbali wamekuja pamoja na kukubaliana maeneo ambayo watasaidia kaunti hii kuwasilisha msaada na kinachoendelea kwa sasa ni kukagua maeneo ambayo yatapewa kipau mbele katika shughuli hiyo.” Alisema Mayeku.