KIWANDA CHA NZOIA GRAINS CHAFUNGULIWA UPYA TRANS NZOIA.

Kiwanda cha kusaga mahindi cha Nzoia Grains Kaunti ya Trans Nzoia kimefunguliwa upya  kuanza kusaga unga utakao anza kuuzwa kwa maduka hivi karibuni, baada ya mgombea wa kiti cha Ugavana Kaunti hiyo  Dk Chris Wamalwa kuingilia kati na kukifufua. 

Akiongea alipozindua kiwanda hicho katika eneo bunge la Endebess mgombea mwenza wa Wamalwa Joyce Cheruto amesema walilazimika kufufua kiwanda hicho kama njia moja ya kuwapiga jeki wakulima akiahidi kuimarisha Sekta hiyo punde tu watakapochukua uongozi. 

Mmoja wa wasimamizi wa kiwanda hicho amemshukuru Wamalwa akisema kiwanda hicho kina uwezo wa kusaga mahindi magunia 120 kwa siku.

Kwa upande wake waziri wa Kilimo Kaunti ya Trans Nzoia Mary Nzomo amesema kiwanda hicho kitakapoimarishwa kitazalisha mapato ya shilingi milioni 42 kila mwezi.

Kiwanda hicho kilichoanzishwa mwaka 2016 kilishindwa kuendelea na shughuli za kawaida kutokana na uongozi duni uliokuwepo.