KITALAWIAN AJIUZULU NA KUTANGAZA KUWANIA UBUNGE SIGOR.


Waziri wa maji, mazingira na mali asili katika kaunti hii ya Pokot magharibi Francis Kitalawian amejiuzulu katika wadhifa huo.
Kitalawian amejiuzulu kulingana na takwa la kisheria ili kuwania kiti cha ubunge cha Sigor katika uchaguzi mkuu ujao huku akisifia utendakazi wake katika kipindi cha miaka minne ambayo amehudumu kwenye wadhifa huo.
Hata hivyo amesema kwa sasa anatarajia kukutana na wakazi wa eneo bunge hilo ambalo kwa sasa linaongozwa Peter Lochakapong ili kupata ushauri kuhusu chama atakacho tumia kuwania wadhifa huo baada ya kile anachodai kutendewa hiana katika chama cha KUP.
Wakati uo huo Kitalawian amemlaumu mbunge wa Pokot kusini David Pkosing kwa kuingilia maswala ya kisiasa ya eneo bunge hilo akitaka wakazi kupewa nafasi ya kufanya maamuzi yao wenyewe kumchagua kiongozi wanayemtaka.
Ikumbukwe katibu katika wizara ya michezo utamaduni na toradhi za kitaifa Simon Kachapin ni miongoni mwa maafisa wakuu katika serikali ya rais Uhuru Kenyatta waliojiuzulu hiyo jana akilenga kuwania kiti cha ugavana katika kaunti hii ya pokot magharibi.