KISA CHA KUPIGWA NG’OMBE RISASI NA POLISI KAINUK CHAZIDI KUKASHIFIWA.


Kisa cha kuuliwa ng’ombe zaidi ya 100 mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Turkana kitendo kinachodaiwa kutekelezwa na maafisa wa polisi kimeendelea kusutwa vikali na viongozi wa matabaka mbali mbali kaskazini mwa bonde la ufa.
Wa hivi punde kushutumu kisa hicho na viongozi wa kidini katika kaunti ya Trans nzoia wakiongozwa kiongozi wa kanisa la PAG nchini Patrick Lihanda ambao aidha waliwataka wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi kuendelea kudumisha amani na kutolipiza kisasi.
“Sisi kama kanisa la PAG Kenya tunahimiza amani kote nchini Kenya. Tunaomba kwamba tuwe na amani kila sehemu na lile tendo ambalo lilifanyika juzi katika kaunti ya Pokot magharibi si zuri kabisa. Wakati huu tuna ukame mkubwa sana nchini na kupoteza mifugo kwa njia hii si vizuri.” Alisema Muhanda.
Muhanda aliitka serikali kufanya uchunguzi kubaini kilichopelekea mifugo hao kuuawa na maafisa wa polisi.
“Kile tunachoomba ni kwamba serikali yetu ifuatilie kwa kina na kuweka wazi kilichotokea kwa sababu tendo hili ni la kikatili.” Alisema.
Wakizungumza katika hafla ya kuzindua jengo jipya la kanisa hilo eneo la Kipsaina kaunti ya Trans nzoia, viongozi hao aidha waliwahimiza wanasiasa kukoma kurushiana cheche za maneno wakisema huenda hali hii ikapandisha joto la kisiasa nchini ikizingatiwa ni miezi michache tu tangu taifa litoke katika msimu wa uchaguzi.
“Tumetoka katika msimu wa siasa. Naomba wanasiasa watulie wakati huu tujenge nchi yetu kwa sababu tuna nchi moja. Tukitupania cheche za maneno yatawasha moto na moto huu ukiwaka itakuwa vigumu sana kuuzima.” Alisema.