KINYANG’ANYIRO CHA USPIKA CHASHIKA KASI POKOT MAGHARIBI
Kinyang’anyiro cha kumtafuta spika wa bunge la kaunti hii ya Pokot magharibi kimeshika kasi huku wagombea 8 wakionyesha nia ya kuwania wadhifa huo.
Miongoni mwa waliotangaza kuwania kiti hicho ni wakili Philip Magal, Fredrick Kaptui Plimo na aliyekuwa mwakilishi wadi ya Chepareria na naibu spika Johson Losilian Kalo.
Wengine ni pamoja na aliyekuwa spika Catherine Mukenyanga ambaye analenga kuhifadhi wadhifa huo pamoja na aliyekuwa katibu wa bunge hilo Julius Kamtoi Ariwoi.
Magal analenga kuwania wadhifa huo akihitaji uungwaji mkono wa wabunge wa chama cha UDA katika bunge hilo sawa na Losilian, huku Mukenyang na Ariwoi wakiegemea chama cha KANU.
Kulingana na Magal, Bunge lililotangulia lilijaa migogoro hali iliyopelekea kutoafikia lolote, na sasa ni wakati bunge hilo linastahili kupata viongozi wenye tajriba.
“Bunge lililotangulia lilisheheni malumbano na mwisho wa siku halikutekeleza lolote huku spika akilaumiwa pakubwa.” Alisema.
Kwa upande wake Kaptui amesema kuwa atatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na wala hatopendelea upande wowote katika kujadili maswala mbali mbali yanayohusu kaunti hii na wakazi kwa jumla.
“Mimi ni mtu mtulivu na mnyenyekevu. Nina imani kwamba niko katika nafasi bora ya kuongoza bunge la kaunti.” Alisema.
Hali hii pia inashuhudiwa katika kaunti ya Trans nzoia wa hivi punde kutangaza kuwania wadhifa huo akiwa wakili Edward Waswa ambaye alielezea jinsi atakavyoimarisha utendakazi wa waakilishi wadi kwa kuwahusisha wote katika maswala ya maendeleo na katika mikutano yote bila ya mapendeleo wala ubaguzi.
Wakati uo huo Waswa alisema atawahusisha waakilishi wadi katika kuandaa warsha mbali mbali za mafunzo ya jinsi wanavyoweza kutekeleza wajibu wao kikamilifu.
Aidha alisema bunge hilo litaongeza fedha za maendeleo kwenye maeneo wadi katika juhudi za kuimarisha maendeleo maeneo ya mashinani.