KINYANG’ANYIRO CHA UBUNGE KAPENGURIA CHAENDELEA KUVUTIA WAGOMBEA ZAIDI.


Chini ya miezi sita kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi agosti, wanasiasa mbali mbali wameendelea kujitokeza kutangaza nia ya kugombea viti vya uongozi katika uchaguzi huo.
Wa hivi punde kutangaza nia yake ni aliyekuwa mwalimu mkuu Jonathan Siwanyang ambaye anagombea kiti cha ubunge eneo bunge la Kapenguria kaunti hii ya Pokot magharibi kupitia tiketi ya chama cha UDA kinachoongozwa na naibu rais William Ruto.
Siwanyang amesema kuwa atatoa kipau mbele kwa maswala ya elimu pamoja na ajira kwa vijana iwapo atapewa fursa ya kuwakilisha eneo bunge hili ambalo kwa sasa linaongozwa na Samwel Moroto ambaye tayari ametangaza kutetea kiti chake kupitia chama chicho hicho cha UDA.
Wakati uo huo Siwanyang ametoa wito kwa vijana katika kaunti hii ya Pokot magharibi kudumisha amani na kutokubali kutumika na wanasiasa kuvuruga amani, akiwahimiza pia wale ambao hawakujisajili kuwa wapiga kura kutumia muda uliosalia kufika katika afisi za IEBC za maeneo bunge ili kufanya hivyo.