KINDIKI ATARAJIWA KUZURU POKOT MAGHARIBI HUKU VISA VYA UVAMIZI VIKITAJWA KUPUNGUA.

Waziri wa usalama na maswala ya ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki anapotarajiwa kurejea katika kaunti ya Pokot magharibi kutathmini hali ya usalama hasa maeneo ya mipakani, wakazi wa kaunti hiyo wamesema kwamba hali ya usalama imeimarika pakubwa.

Wakiongozwa na Joseph Lokiranyang, wakazi hao walisema kwamba tangu oparesheni ya kuwakabili wahalifu ilipoanzishwa maeneo hayo ya mipakani, visa vya wizi wa mifugo na kuuliwa kiholela wakazi wa maeneo hayo vimepungua pakubwa.

Hata hivyo wakazi hao walimtaka waziri Kindiki kuwapa uhamisho maafisa wa usalama ambao wamedumu katika kaunti hiyo kwa miaka mingi ili kuimarisha huduma za idara ya polisi.

“Tangu oparesheni ya usalama kuwakabili wahalifu maeneo ya mipakani mwa kaunti hii kuanzishwa, visa vya uvamizi vimepungua pakubwa. Waziri Kindiki anapokuja kaunti hii tunaomba kwamba atafakari kuhusu kuwahamisha maafisa wa usalama ambao wamedumu miaka mingi kaunti hii ili kuimarisha huduma ya polisi.” Walisema.

Wakati uo huo wakazi hao waliitaka serikali kuimarisha miundo msingi eneo la Lami Nyeusi mpakani pa kaunti hiyo na kaunti ya Turkana ili kuimarisha doria ya maafisa wa usalama na kuwawezesha wakazi wa eneo hilo kuendeleza shughuli zao bila kutatizwa na wahalifu.

“Tunaomba serikali kuimarisha miundo msingi eneo la Lami nyeusi ikiwa ni pamoja na kujenga barabara ili kuwasaidia maafisa wa polisi kuimarisha doria na kuwawezesha wakazi wa maeneo hayo kuendelea na shughuli zao bila ya kuwa na wasi wasi wa kuvamiwa na wahalifu.” Walisema.