KINDIKI ATAKIWA KUFANIKISHA KUPANDISHWA VYEO MACHIFU WALIOONGEZA MASOMO.

Gavana wa kaunti ya Elgeyo marakwet Wesley Rotich ametoa wito kwa waziri wa usalama wa ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki kuhakikisha kwamba machifu ambao waliongeza masomo wanapandishwa vyeo na kuwa wasaidizi wa kamishina.

Akizungumza katika hafla moja eneo la Kamelei mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na Elgeyo marakwet, Rotich alisema kwamba hatua hiyo itawapa motisha wakuu hao wa usalama kutekeleza majukumu ya kuhakikisha kwamba wahalifu wanaosababisha utovu wa usalama mpakani pa kaunti hizi wanakabiliwa.

“Wapo machifu wetu hapa katika kaunti za Pokot magharibi na Elgeyo marakwet ambao wameongeza masomo na kupata shahada. Tunaomba kwamba waziri wa usalama Kithure Kindiki awapandishe vyeo na kuwa wasaidizi wa kamishina ili wawe na motisha ya kufanya kazi.” Alisema Rotich.

Wakati uo huo Rotich alipongeza ushirikiano uliopo baina ya wakazi wa kaunti hizi na maafisa wa usalama katika kukabili watu wanaoshukiwa kuwa wezi wa mifugo hatua aliyosema kwamba inasaidia pakubwa juhudi za kukabili uhalifu huo kanda hii.

“Sasa hivi tumeimarisha ushirikiano baina ya wananchi na maafisa wa polisi ambapo mtu yeyote ambaye anashukiwa kuwa mwizi, anakamatwa na kuwasilishwa kwa maafisa wa usalama. Hali hii imesaidia kupunguza visa vya wizi wa mifugo maeneo haya.” Alisema.

[wp_radio_player]