KINDIKI ALAUMIWA KUFUATIA MAUAJI YA MTU MMOJA LAMI NYEUSI.

Viongozi kaunti ya Pokot magharibi wamelaani vikali kisa cha kuuliwa mtu mmoja eneo la Lami nyeusi na wavamizi wanaoaminika kutoka kaunti jirani.

Wakiongozwa na naibu gavana kaunti hiyo Robert Komole, viongozi hao walimlaumu waziri wa maswala ya ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki kwa kutotekeleza ahadi ya kuajiri maafisa wa akiba NPR upande wa pokot magharibi huku kaunti jirani zikiwa na maafisa hao.

“Tunalaani kabisa kisa cha hapo jana ambapo mtu mmoja aliuliwa kwa risasi eneo la lami nyeusi na watu wanaoaminika kutoka kaunti jirani.. Mimi namlaumu waziri Kindiki kwa sababu tuliomba maafisa wa NPR kaunti hii lakini hadi sasa hamna hatua ambayo imechukuliwa.” Alisema Komole.

Komole alidai kwamba hatua ya kuwahami maafisa wa NPR katika kaunti jirani imepelekea swala la usalama kuwa tete hasa upande wa Pokot magharibi, akidai huenda bunduki iliyotumika katika mauaji hayo ni ya afisa wa NPR kutoka kaunti jirani.

“Inasemekana bunduki iliyotumika kumwua mtu huyu ni ya afisa wa NPR. Haya ndio matokeo ya kuwahami maafisa hawa upande mmoja na kuutelekeza upande mwingine.” Alisema.

Alitoa wito kwa vitengo vya usalama kufuatilia bunduki iliyotumika kutekeleza mauaji hayo na kumtia nguvuni mmiliki wake.

“Ningeomba vitengo vya usalama kufuatilia kitendo hicho kwa sababu sasa inajulikana kwamba risasi hiyo ni ya NPR. Sasa ni rahisi kujua ni bunduki ya afisa gani ilitumika. Wafuatilie bunduki hiyo na afisa huyo akamatwe na kufunguliwa mashitaka.” Alisema.