KINA MAMA WATAKIWA KUJIHUSISHA NA KILIMO NA KUTOWATEGEMEA ZAIDI WAUME ZAO KWA KILA JAMBO.
Kina mama katika kaunti ya Pokot magharibi wametakiwa kujihusisha na swala la kilimo cha ufugaji ili waweze kujikimu kimaisha na kutotegemea zaidi waume zao kwa kila jambo.
Akizungumza eneo la Kacheliba katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo iliambatana na siku ya chakula duniani, mkewe gavana Scovia Kachapin aidha aliwataka kina mama kutotumia mazao yanayotokana na kilimo chao kwa maswala ya kifedha tu, bali pia watumie kama chakula kwa afya bora.
Wakati uo huo Bi. Kachapin alisema serikali ya kaunti chini ya uongozi wa gavana Simon Kachapin ipo mbioni kuboresha maisha ya kina mama kwa kuwapa njia mbadala za kupata mapato licha ya kiangazi kikali kinachokumba eneo hilo.
“Tunawahimiza kina mama kwamba waweze kuwa na sehemu ambazo wamepanda mboga zao na kujihusisha pia na ufugaji wa kuku na mbuzi, ili panapotokea hitaji wauze na kugharamia mahitaji hayo bila kuwategemea zaidi waume zao.Pia wasitumie tu mazao yao kwa ajili ya kifedha bali pia waweze kula ili wawe na afya bora.” Alisema Scovia.
Kauli yake ilitiliwa mkazo na waziri wa kilimo kaunti ya Pokot magharibi Wilfred Longronyang ambaye aidha aliwataka kina mama kuzingatia pakubwa lishe bora hatua ambayo pia itasaidia kukabili swala la utapia mlo miongoni mwa watoto.
“Kina mama pia waweze kuzingatia sana lishe bora ili tuweze kukabili swala utapia mlo miongoni mwa watoto ambao hutokana na ukosefu wa lishe bora.” Alisema Longronyang.