KIMACHAS: TUTAFANYA KILA JUHUDI KUHAKIKISHA MTAALA WA CBC UNAFAULU.
Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kutosha kuhakikisha kwamba mtaala mpya wa elimu CBC unafanikiwa.
Akizungumza afisini mwake Mkurugenzi wa tume ya huduma kwa walimu TSC kaunti ya Pokot magharibi Benard kimachas alisema tayari walimu 629 wameajiriwa huku wengine 112 wanaofunza shule za msingi wakipokea mafunzo ya kuwahudumia wanafunzi wa sekondari ya msingi.
“Tulipewa walimu 629 wa kuajiri, na tumewaajiri wote. Tumechukua pia wale ambao wanafunza katika shule za msingi kusaidia katika shule za sekondari ya msingi na pia tunaendelea kuwafunza wengine ili kufanikisha mtaala huu.” Alisema Kimachas.
Aidha Kimachas alisema tume hiyo imetuma walimu katika shule zote kwenye maeneo ambayo yanakabiliwa na utovu wa usalama, akiwahakikishia wazazi kwamba masomo yanaendelea kwenye shule hizo chini ya ulinzi mkali.
“Kwa sasa shule zote ambazo tulifaa kuwatuma walimu, tumekwishawatuma hata, zile ambazo ziko katika maeneo ambayo yanashuhudia utovu wa usalama na wanaendeleza shughuli zao chini ya ulinzi wa maafisa wa polisi.” Alisema.
Wakati uo huo Kimachas alitaja ndoa za mapema na kukeketwa, kuwa changamoto kuu kwa elimu ya mtoto wa kike kwenye maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo hasa maeneo ya mipakani na taifa jirani la Uganda.
“Kaunti hii ina changamoto kadhaa ambazo watoto wetu wa kike bado wanakabiliana nazo. Kuna changamoto kama kuozwa mapema pamoja na kuwakeketa hasa maeneo ya mipakani pa kaunti hii na taifa la Uganda.” Alisema.