KIJANA MMOJA ENEO LA KAIBOS AUMIZWA SEHEMU NYETI NA MAAFISA WA POLISI WA KITUO CHA KAIBOS KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI
Familia moja eneo bunge la Kapenguria kaunti hii ya Pokot magharibi inalilia haki kufuatia madai ya jamaa yao kukamatwa na kudhulumiwa na maafisa watatu wa polisi wa kituo cha Kaibos kufuatia deni la shilingi 100.
Jamaa za mwathiriwa Barnabas Kiptoo mwenye umri wa miaka 21 wameandamana wakibeba mabango wakidai kuwa mwathiriwa alijeruhiwa vibaya na polisi hao hali iliyompelekea kulazwa katika hospitali ya mafunzo na rufaa mjini Eldoret kwa upasuaji.
Akizungumza na wanahabari mwathiriwa amesema kuwa alikamatwa na maafisa hao tarehe 11 mwezi aprili na maafisa hao ambao walimdhulumu vibaya akiwa katika seli za polisi mmoja wao akimkanyaga kifuani, na kisha mwingine kutumia pingu kumjeruhi vibaya sehemu zake nyeti hali iliyompelekea kupiga kamsa na kuwavutia watu waliokuwa karibu kushuhudia kichokuwa kikijiri.
Kulingana na Kiptoo maafisa hao waliagiza akimbizwe katika hospitali ya Kapenguria kupewa matibabu baada ya kugundua kuwa wamemjeruhi vibaya ambapo baadaye alipelekwa katika hospitali ya rufaa ya Eldoret ambako iligundulika kuwa alijeruhiwa vibaya sehemu zake nyeti ambazo zilikuwa zimeanza
Kuoza hali iliyolazimu kuondolewa baadhi ya sehemu hizo.
Familia ya mwathiriwa imelaani vikali kitendo hicho wakisema kuwa mwanao sasa ameharibiwa maisha yake huku wakitoa wito kwa haki kutendeka kwa mpendwa wao.
Ni kisa ambacho pia kimeshutumiwa vikali na afisa wa mipango katika shirika la centre against torture Kimtai Kirui akisema mamlaka ya kuangazia utendakazi wa polisi IPOA inachunguza kisa hicho akielezea matumaini ya haki kutendeka.
Ni kauli ambayo imesisitizwa na kamanda wa polisi kaunti ya Pokot magharibi Jackson Tumwet ambaye amethibitisha kutukia kisa hicho akisema kuwa pia anendesha uchunguzi kubaini kilichotokea.