KICD YATETEA HATUA YA KUWEKA LUGHA YA POKOT CHINI YA JAMII YA KALENJIN.


Taasisi ya mitaala nchini KICD imetetea hatua yake ya kuweka lugha ya pokot chini ya jamii ya kalenjin katika hatua ya kujumuisha lugha za kiasili kwenye mtaala wa elimu nchini kwa wanafunzi hasa wanaoanza masomo chini ya mtaala mpya wa elimu.
Ikijibu barua ya seneta wa kaunti hii ya pokot magharibi Samwel Poghisio ambaye aliiandikia akilalamikia hatua hiyo, KICD imesema kuwa ilichukua hatua hiyo kwa kuwa haikupokea michango kutoka kwa lugha nyingi za kiasili ikiwemo ya kipokot hivyo ikawa vigumu kuiweka kama lugha inayojisimamia.
Katika barua iliyoandikwa tarehe tatu mwezi huu wa agosti, KICD imetoa wito wa michango kuhusu lugha ya pokot kuwasilishwa ili kufanikisha juhudi za kuandaa mtaala utakaowezesha kujumuishwa lugha za kiasili katika mtaala wa elimu nchini.
Katika barua yake iliyoandikwa tarehe mosi mwezi july, Poghisio alilalamikia hatua ya lugha ya pokot kujumuishwa katika lugha za jamii ya kalenjin hali aliyosema huenda ingemnyima mtoto wa kipokot haki ya kupata elimu akisema kuwa pokot ni lugha inayojisimamia na inalindwa chini ya makubaliano ya umoja wa mataifa kuhusu lugha za kiasili.