KENYATTA ASUTWA KWA KUENDELEA KUJIHUSISHA NA SIASA LICHA YA KUSTAAFU.

Kauli ya rais mustaafu Uhuru Kenyatta katika mkutano wa wajumbe wa chama cha jubilee kwamba hatang’atuka katika uongozi wa chama hicho hadi wajumbe wake watakapoamua hivyo, imeendelea kuibua hisia mseto kutoka kwa wakenya.

Baadhi ya wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi wakiongozwa na Henry Sonko wamesema kwamba hatua ya Kenyatta kuendelea kushikilia uongozi wa chama hicho haihusiani na nia ya kuendelea kukiongoza bali kukitumia kama ngao dhidi ya mashambulizi kutoka kwa mahasimu wake.

Walisema kwamba Kenyatta anafahamu fika kwamba iwapo ataamua kustaafu kabisa kutoka kwenye siasa na uongozi wa chama hatakuwa na njia yoyote ya kujitetea kutokana na madai ambayo yanaibuliwa dhidi yake hasa kutoka upande unaomuunga rais William Ruto.

“Uhuru hawezi kustaafu sasa hivi kwa sababu anajua kwamba iwapo ataachilia wadhifa wa kiongozi wa jubilee hamna jinsi ambavyo tajitetea kuhusiana na shutuma ambazo zinaelekezwa kwake kutoka kwa mrengo wa rais Ruto. Sasa anatumia jubilee kama ngao dhidi ya mashambulizi ya mahasimu wake kisiasa.” Walisema.

Wakazi hao sasa wanatoa wito kwa Kenyatta kutunza heshima yake kama rais mustaafu kwa kustaafu rasmi kutoka siasani na kumwachia kinara wa azimio Raila Odinga majukumu ya kuiwajibisha serikali ya rais William Ruto.

Wamedai kwamba hatua ya Kenyatta kuendelea kung’ang’ania uongozi wa chama inashusha hadhi yake kama rais mustaafu.

“Yeye kama kiongozi aliyeheshimika, amekuwa rais katika taifa hili kwa miaka kumi, anafaa kujiheshimu na kustaafu kutoka siasani. Maswala ya upinzani anafaa kumwachia kinara wa azimio Raila Odinga kwa sababu yeye ndiye kiongozi wa upinzani.” Walisema.

Ikumbukwe katika mkutano wa wajumbe wa chama cha Jubilee jumatatu iliyopita, Kenyatta aliapa kutostaafu kama kiongozi wa chama hicho kufuatia shinikizo zinazotoka kwa wanachama wanaoegemea mrengo wa mbunge wa bunge la Afrika mashariki EALA Kanini Kega.

Aidha kika hicho kilitumika kuwatimua chamani Kega pamoja na mbunge mteule Sabina Chege kwa kukiuka sheria za chama na kujihusisha na serikali ya Kenya kwanza, licha ya Jubilee kuwa chama tanzu cha muungano wa azimio la umoja one Kenya.