KENYA SEED YATOA MSAADA WA VISODO KWA AJILI YA WANAFUNZI TRANS NZOIA.


Kama njia moja ya kuhakikisha mtoto wa kike anasalia shuleni bila ya matatizo ya kukosa taulo za hedhi, Kampuni ya uzalishaji mbegu Kenya seed imetoa msaada wa laki moja kwa shirika moja linalo shughulikia watoto wa kike,wajane na wasiojiweza katika jamii kwa jina Giving hope to the society, kupiga jeki shughuli za kutoa visodo watoto wa kike wanaporejea shuleni juma lijalo.
Kwenye mkao na wanahabari baada ya kutoa hudi hiyo, mkurugenzi wa Kenya seed Fred Oloibei amesema wamechukua hatua hiyo kama njia ya kurudisha shukrani kwa wenyeji wa Sirende na eneo bunge la Kiminini kwani ni washirika wakuu wa kampuni hiyo ya mbegu nchini.
Aidha Oloibei amesema hatua hiyo itasadia kuwaepusha wasichana hao dhidi ya hatari za mimba na ndoa za mapema, hivyo kutoafikia ndoto yao maishani kutokana na ugumu wa kiuchumi kwa wazazi wao baada ya kuzuka kwa janga la covid 19.
Wakati huo huo Oloibei ametoa wito kwawenyeji eneo hilo kukumbatia mbegu za Kenya seed kwani zimethibitishwa kuwa na ubora wa hali ya juu hivyo kusaidia serikali katika kuafikia moja wapo ya ajenda kuu ya utoshelezaji wa chakula nchini.