KEMSA yaipokeza kaunti ya Pokot magharibi dawa za kima cha shilingi milioni 60

Na Benson Aswani,
Huduma za matibabu zinatarajiwa kuimarika katika hospitali mbali mbali katika kaunti ya Pokot magharibi baada kupokezwa dawa ya kima cha shilingi milioni 60 kutoka kwa shirika la kusambaza dawa na vifaa vya matibabu KEMSA.
Akizungumza wakati akipokea dawa hizo katika hospitali ya Kapenguria, naibu gavana Robert Komole alisema licha ya kaunti hiyo kuitisha dawa za kima cha shilingi milioni 65, imepokezwa dawa za kima cha shilingi alfu 60,hatua aliyosema imetokana na rekodi nzuri ya kulipa madeni yake kwa shirika hilo.
“Tumesikilizwa leo na watu wa KEMSA. Tuliitisha dawa za shilingi milioni 65 ila KEMSA imetupa za kima cha shilingi milioni 60. Tunashukuru kwa sababu KEMSA imeweza kutuamini kutokana na historia nzuri ambayo tuko nayo kwa shirika hilo katika kulipa madeni,” alisema Komole.
Waziri wa afya kaunti hiyo Cleah Parklea alisema dawa hizo zitasambazwa kwenye zahanati zote 158 katika kaunti hiyo ya Pokot magharibi, akitoa wito kwa wasimamizi wa zahanati hizo kuhakikisha usimamizi bora wa dawa ili ziweze kwasaidia wananchi.
“Dawa hizi zinaenda kwa zahanati zetu 158. Na nawaomba wasimamizi wa vituo vyote ambavyo vitapokea dawa hizi kuhakikisha kwamba zinatumika vyema ili ziwasaidie watu wetu wanaotafuta huduma za matibabu,” alisema Parklea.
Kwa upande wake msimamizi wa KEMSA eneo la kaskazini mwa bonde la ufa zaccheus Muya alitoa hakikisho kwa wakazi wa kaunti hiyo kwamba dawa zilizosalia za kima cha shilingi milioni 5 zitasambazwa hivi karibuni.
“Mmesikia kwamba tumeleta dawa za shilingi milioni 60. Ukweli ni kwamba tulipokea maombi ya dawa za kima cha shilingi milioni 65. Mtu anawezajiuliza kwamba na zilizosalia itakuwaje? Hizi dawa ambazo zimesalia za kima cha shilingi milioni 5 zitakuja hivi karibuni,” alisema Muya.