‘KELELE’ ZA KINDIKI ZAONEKANA KUTOYUMBISHA NAFSI ZA WAVAMIZI BONDE LA KERIO.


Washukiwa wa wizi wa mifugo wamevamia vijiji vya Lokwar, Nakuse na Kaptir Turkana kusini kaunti ya Turkana na kuwaua wanafunzi wanne huku mamia ya wakazi wakilazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na utovu wa usalama.
Ni uvamizi unaojiri takriban siku tatu tu baada ya waziri wa usalama wa ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki kuzuru eneo la Lokichogio na Nadapar kaunti ya Turkana kutathmini hali ya usalama, na kuahidi kuwatuma maafisa zaidi wa usalama na maafisa wa NPR kusaidia kurejesha usalama maeneo hayo.
Wakazi wa meneo hayo walimlaumu waziri Kindiki kwa kile walidai kuyakimbilia maeneo yaliyo salama huku maeneo ambayo yanakabiliwa na hatari ya uvamizi yakikosa kuangaziwa.
“Waziri Kindiki amekuwa hapa Turkana na badala ya kuja sehemu ambazo zimeathirika anaenda sehemu ambazo zina amani. Hapa kuna mambo mabaya ambayo yanafanyika, na nafahamu kwamba aliko anajua Turkana south kuna shida.” Walisema.
Kamishina wa kaunti ya Turkana Jacob Ouma amewahakikishia kwamba wahalifu hao watasakwa na kukabiliwa kama majambazi akisema kwamba kamwe hawatakuwa na huruma na mtu yeyote ambaye anahatarisha maisha ya wakazi.
“Hatutakubali tena tabia ya watu fulani kuja kuvuruga amani ya watu katika maeneo yao. Tutawasaka hawa wahalifu na kuhakikisha kwamba wanakabiliwa.” Alisema Ouma.