KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI YA POKEA DAWA ZA KIMA CHA SHILINGI MILIONI 49.9 KUTOKA KEMSA.
Huduma za matibabu katika hospitali za kaunti ya Pokot magharibi zinatarajiwa kuimarika zaidi baada ya serikali ya kaunti kupokea dawa za kima cha shilingi milioni 49, 900 alfu, 916 kutoka kwa shirika la kusambaza dawa na vifaa vya matibabu nchini KEMSA.
Akizungumza wakati wa kupokea rasmi dawa hizo, waziri wa afya kaunti Cleah Parklea alisema kwamba zitasambazwa katika vituo vyote vya afya kwa usawa, huku akikashifu vikali taarifa ambazo zimeenezwa katika mitandao ya kijamii kwamba vituo vya afya kaunti hiyo havina dawa za kutosha.
“Hizi lori saba zimebeba dawa zinazogharimu shilingi milioni 49,900,916, na zinaenda katika vituo 145 vya afya kaunti hii ya Pokot magharibi. Tunawahakikishia wananchi kwamba dawa hizi zitasambazwa kwa usawa katika vituo hivi. Pia nakanusha madai kwamba vituo vyetu vya afya havina dawa. Huo ni uongo mtupu.” Alisema Parklea.
Afisa katika shirika la KEMSA Zacheus Muya alipongeza ushirikiano bora ambao umekuwepo baina ya kaunti hiyo na shirika hilo unaohusisha kuagiza na kulipia kwa wakati dawa hizo, akisema kwamba umerahisha pakubwa shughuli zake.
“Kaunti hii ya Pokot magharibi ni ya kipekee sana katika rekodi zetu za KEMSA. Kwa sababu ikija katika kuagiza dawa, huagiza kwa wakati na hatuna deni na kaunti hii.” Alisema Muya.
Kwa upande wake mkurugenzi wa idara ya afya kaunti hiyo Dkt. Jacob Ruto alisema hatua hii itarahisisha shughuli za matibabu kwa wananchi maeneo mbali mbali, akiwataka wasimamizi wa vituo vya afya kuhakikisha zinatumika vyema, kauli ambayo ilisisitizwa na afisa anayesimamia dawa kaunti hiyo Dkt. Korir.
“Itakuwa rahisi sana kwa watu wetu kupata huduma za matibabu kwa kuwepo dawa za kutosha. Tungependa kutoa wito kwa wahudumu wa afya katika vituo vyote vya afya kaunti hii kuhakikisha kwamba dawa hizi zinatumika vyema ili kuwafaidi watu wetu kiafya.” Walisema.