KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI HATIMAYE YAPEWA MAAFISA WA NPR BAADA YA SHINIKIZO ZA MUDA.

Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameipongeza serikali kupitia wizara ya usalama na maswala ya ndani ya nchi kwa kuhakikisha kwamba kaunti hiyo pia inapewa maafisa wa akiba NPR hatua ambayo imekuwa ikishinikizwa kwa muda sasa na viongozi.

Akizungumza katika mahojiano na kituo hiki, gavana Kachapin alisema kwamba hatua hii itasaidia pakubwa katika kuhakikisha kwamba maeneo ambayo yamekuwa yakikabiliwa na utovu wa usalama hasa mipakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani za Turkana na Elgeyo Marakwet yanashuhudia amani.

Aidha Kachapin alielezea imani kwamba shughuli za masomo zitarejelewa mwezi januari katika shule ambazo zilifungwa maeneo hayo ya mipakani kutokana na utovu wa usalama.

Serikali kuu imetupa sasa hao maafisa wa NPR ambao tumekuwa tukishinikiza kwa muda, na mimi kama gavana nashukuru kwa hilo. Naamini kwamba sasa swala la utovu wa usalama litashughulikiwa na kuhakikisha shule zilizofungwa zinarejelea shughuli za masomo mwezi januari.” Alisema Kachapin.

Kachapin alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakazi wa kaunti hiyo kuwa na subira wakati serikali inaposhughulikia swala zima la usalama, huku pia akiwataka wanasiasa kutotumia swala la usalama kuendeleza siasa zao za uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

“Nawahimiza watu wetu kuwa watulivu wakati huu abapo serikali inaendelea kushughulikia usalama, nikitoa wito kwa wanasiasa pia kukoma kutumia swala la usalama  kuendeleza siasa zao za uchaguzi mkuu ujao.” Alisema.