KAUNTI YA ELGEYO MARAKWET YAENDELEA KUWEKA MIKAKATI YA KUKABILI UKEKETAJI


Serikali ya kaunti ya Elgeyo Marakwet kwa ushirikiano na shirika la umoja wa mataifa kuhusu idadi ya watu, serikali ya kitaifa na shirika la Marakwet girls foundation, imefanya mashauriano kuhusu namna ya kukomesha ukeketaji katika kaunti hiyo.
Mashauriano hayo ambayo yalifanyika eneo la Chesongoch yalilenga kuwafahamisha wakazi kuhusu athari za ukeketaji na kupata njia bora ya kukomesha tamaduni hiyo hasa katika eneo la marakwet mashariki.
Afisa kutoka shirika hilo la umoja wa mataifa Ademola Olajide amesema shirika hilo linalenga kudumisha na kulinda haki za wasichana na kina mama dhidi ya ukeketaji.
Waziri wa huduma,vijana, jinsia na jamii katika kaunti hiyo kiprono Chepkok amesema kupitia mazungumzo hayo itawapa wakazi ufahamu kuwa ukeketaji ni mila ambayo imepitwa na wakati na yenye madhara mengi hasa kwa watoto wa kike.