KATAMA: USALAMA UMEIMARIKA BAADA YA KUAJIRIWA MAAFISA WA NPR.

Maafisa wa NPR.

Na Emmanuel oyasi.

Idara ya usalama katika kaunti ya Pokot magharibi imewahakikishia wakazi wa maeneo ya mipakani ambayo yamekuwa yakishuhudia utovu wa usalama kwamba hali ya usalama imeimarishwa maeneo haya baada ya kuajiriwa rasmi maafisa wa akiba NPR.

Kamanda wa polisi kaunti hiyo Peter Katam alisema kwamba maafisa hao tayari wametumwa maeneo ya mipakani pa kaunti hiyo na kaunti jirani za Elgeyo marakwet, Turkana na taifa jirani la Uganda ambako kumekuwa kukishuhudiwa visa hivyo kwa wingi shule zikipewa kipau mbele.

Aidha Katam aliwahimiza wakazi wa maeneo hayo kushirikiana na maafisa wa usalama kwa kutoa ripoti kwa wakati wanaposhuhudia kisa chochote cha utovu wa usalama, ambao unasababishwa na wezi wa mifugo ili kuhakikishiwa usalama wao.

“Usalama umeimarika maeneo ya mipakani kwani tayari tumewatuma maafisa wa NPR walioajiriwa majuzi katika maeneo mbali mbali ambayo yalikuwa na changamoto, tukizingatia zaidi shule. Nawahimiza wananchi kushirikiana na maafisa wa usalama kunapotokea kisa chochote cha utovu wa usalama.” Alisema Katam.

Katam alisema shughuli za masomo katika shule za maeneo hayo zimeanza kurejelewa japo kwa upole akiwahimiza wazazi kuwapeleka wanao shuleni hasa baada ya masomo kuathirika maeneo hayo kufuatia utovu wa usalama, ili pia wakaweze kunufaika na masomo kama wenzao maeneo mengine ya nchi.

“Wanafunzi wamerejea katika shule ambazo zilikuwa zimefungwa japo kwa upole. Tunawahimiza wazazi kuhakikisha kwamba watoto wao wanarejea shule ili pia wakaweze kupata elimu, kwani sasa kuna usalama wa kutosha.” Alisema.

Aliwataka wote wanaomiliki bunduki kinyume cha sheria kuzirejesha, akionya kwamba hatua zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayepatikana nayo wakati wa msako.