KASHEUSHEU: SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI NDIYO INAYOTENGA KIWANGO KIKUBWA CHA PESA ZA BASARI.
Mwakilishi wadi maalum Elijah Kasheusheu ameelezea kujitolea kwa serikali ya gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin katika kuimarisha sekta ya elimu.
Kasheusheu alisema kwamba ni serikali ya gavana kachapin pekee ambayo imetenga kiwango kikubwa cha fedha ambazo zinatumika kwa ajili ya basari, ambacho kinawezesha idadi kubwa ya wanafunzi kaunti hiyo kutoka jamii zisizojiweza kupata elimu.
Aidha Kasheusheu alisifia serikali ya gavana Kachapin kwa kuzingatia uwazi katika kutoa fedha hizo za basari ikilinganishwa na serikali ya awali.
“Sisi tunajua kwamba gavana ameongeza kiwango cha fedha za basari kwa sababu sisi tuko kwenye bunge. Katika taifa zima la Kenya, ni kaunti hii ya Pokot magharibi pekee ambayo imetenga fedha nyingi za basari.” Alisema Kasheusheu.
Kauli yake Kasheusheu ilifuatia ombi la chama cha walimu wa shule za upili na vyuo vya kadri KUPPET tawi la kaunti ya Pokot magharibi kwa gavana Kachapin kuendeleza mpango wa kutoa fedha hizo shule zitakapofunguliwa mwezi januari mwakani.
“Kama miungano ya walimu tunatambua kazi ya gavana Kachapin kwa maswala ya elimu. Ila kile ambacho tunaomba ni kwamba, mpango wa kutoa fedha za basari uendelee mwaka ujao ili wanafunzi waweze kuendelea na masomo bila kutatizika.” Walisema.