KASHEUSHEU ATETEA HATUA YAKE YA KUHAMA KANU NA KUJIUNGA NA UDA.


Mwakilishi wadi maalum kaunti hii ya Pokot magharibi Elijah Kasheusheu ametetea vikali hatua yake ya kughura chama cha KANU na kujiunga na chama cha UDA ambacho kinaongozwa na naibu rais William Ruto.
Akizungumza katika mahojiano na kituo hiki muda mfupi uliopita, kasheusheu amesema kuwa aliamua kuchukua hatua ya kujiunga na UDA kutokana na sera yake ya kumjali pakubwa mwananchi wa viwango vya chini, pamoja na kusikiliza matakwa ya wakazi wa wadi ya mnagei ambako anatarajia kugombea kiti cha mwakilishi wadi katika uchaguzi mkuu ujao.
Hata hivyo Kasheusheu amesema kuwa kwa sasa ataendelea kutekeleza majukumu yake kama mwakilishi wadi maalum wa chama cha KANU hadi kitakapokamilika kipindi chake cha kuhudumu na kugombea kiti cha mwakilishi wadi ya mnagei kupitia UDA.
Wakati uo huo Kasheusheu amekashifu mwafaka baina ya rais Uhuru Kenyatta na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga akidai kuwa ulipelekea kutengwa baadhi ya viongozi hasa wale ambao wanaegemea mrengo wa naibu rais William Ruto.