KANU YAWAONYA WANACHAMA WAKE DHIDI YA KUSHIRIKI MCHAKATO WA KUMBANDUA SPIKA WA BUNGE LA POKOT MAGHARIBI.


Chama cha KANU kimewaonywa wabunge wa bunge la kaunti hii ya pokot magharibi wanachama wa chama hicho dhidi ya kushiriki mchakato wa kumbandua afisini spika wa bunge la kaunti hii Catherine Mukenyang.
Katika barua iliyoandikwa na kutiwa sahihi na katibu mkuu wa kitaifa wa KANU Nick Salat, chama hicho kimeonya kuwa mwanachama yeyote wa Kanu katika bunge hilo atakayeshiriki mchakato huo atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Chama hicho kimewataka wanachama wake kuzingatia katiba ya chama ambayo waliapa kutii kabla ya kuidhinishwa kutumia tiketi yake na kujitenga na swala hilo, kwani chama hakijapata misingi yoyote ya kubanduliwa afisini spika Mukenyang.
Ikumbukwe hoja ya kubanduliwa spika Mukenyang iliwasilishwa na mwakilishi wadi ya Endough Evanson Lomaduny kwa misingi ya utumizi mbaya wa afisi, kukiuka maadili ya utendakazi, kwenda kinyume na katiba katika utendakazi wake miongoni mwa tuhuma nyingine.
Hata hivyo mukenyang alipinga madai yaliyoibuliwa dhidi yake akisema kuwa hatua hiyo ilichochewa kisiasa huku akidai wapo baadhi ya waakilishi wadi ambao wamekiri kushurutishwa na baadhi ya viongozi kaunti hii ya Pokot magharibi kutia saini ya kubanduliwa kwake afisini.