KANISA LA ST. ANDREWS ACK KAPENGURIA LAENDELEA KUKUMBWA NA MZOZO WA UONGOZI.

Kanisa la kianglikana la St. Andrews dayosisi ya Kapenguria limeendelea kukumbwa na mzozo wa uongozi ambao umetatiza ibaada hapo jana waumini wakilalamikia mbinu inayotumika kuchagua uongozi wa kanisa hilo.

Wakiongozwa na Jackson Kakuko ambaye ni mmoja wa wazee wa kanisa hilo, waumini hao walilalamikia kukiukwa kwa katiba ya kanisa hilo wakidai kamati ambayo ilibuniwa kuongoza dayosisi hiyo haikufuata utaratibu unaohitajika kulingana na katiba ya kanisa.

“Uongozi wa kanisa hili unajaribu kutulazimishia kamati ya mpito kabla yetu kupata askofu katika kanisa hili. Sisi hatutakubali katiba ya kanisa kukiukwa. Hatutakubali kulazimishiwa viongozi kupitia njia ya mkato. Mchakato wa kumchagua askofu unafaa kuanzishwa na kamati iliyobuniwa kikatiba.” Walisema waumini.

Aidha waumini hao walidai uongozi wa kanisa hilo umeleta migawanyiko kwa kuonyesha upendeleo katika mchakato mzima wa kumchagua askofu, kwa kutumia mbinu ya kupaka tope upande mmoja ili mtu wanayependelea kuwa askofu apate nafasi hiyo.

“Hawa viongozi hawakuja kuleta waumini wa kanisa hili pamojha ila kuleta migawanyiko, kwa sababu wanaonyesha upendeleo kwa pande mbili ambazo zinawania nafasi hii. Wanawapaka tope kundi moja kwa kupendelea kundi ambalo wanataka litwae uongozi wa kanisa hili.” Walisema.

Mzozo huo ulipelekea kuathirika ibaada ya jumapili ambapo waumini walilazimika kuendesha ibaada nje baada ya kanisa hilo kufungwa huku baadhi ya waumini wakishutumu vikali tukio hilo ambalo walilitaja kuwa kinyume cha maadili ya kikristo.

“Sisi wakristo wengi hatupendi haya mambo ambayo tumeyashuhudia leo. Sisi tunataka watu wawe pamoja kwa sababu mambo kama haya ni kinyume cha maadili ya kikristo.” Walisema.