KAMATI YA ELIMU KATIKA BUNGE LA POKOT MAGHARIBI YATOA HAKIKISHO LA KUTOLEWA MAPEMA FEDHA ZA BASARI.

Kamati ya elimu katika bunge la kaunti ya Pokot magharibi imetoa hakikisho kwa wanafunzi na wazazi katika kaunti hiyo kwamba fedha za basari zitatolewa kabla ya tarehe 19 mwezi januari ili kuwaruhusu wanafunzi kuendelea na masomo bila ya changamoto yoyote.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni mwakilishi wadi ya Siyoi Esther Serem alisema kwamba kwa sasa wanachama wa kamati ya basari wanaendeleza ukusanyaji wa data katika wadi zote baada ya kukamilika makataa ya kutuma maombi kwa wanaohitaji basari.

“Tunalenga kuhakikisha kwamba fedha za basari zimepeanwa katika shule za kaunti hii kufikia tarehe 19 mwezi januari. Kwa sasa kamati ya basari inaendeleza ukusanyaji wa data katika wadi zote baada ya makataa ya kutuma maombi kukamilika.” Alisema Serem.

Hata hivyo Serem aliwahimiza wazazi kutekeleza jukumu lao la kulipia sehemu ya karo itakayosalia kwani fedha za basari hazigharamii karo yote ya wanao.

Aliwataka wazazi kutotumia fedha zote katika sherehe za krismasi na mwaka mpya na badala yake kuwa waangalifu katika matumizi ya fedha ili kuwalipia wanao karo shule zitakapofunguliwa mwezi januari mwaka ujao.

“Nawahimiza wazazi kuwa makini wanaposherehekea msimu huu wa krismasi na mwaka mpya. Wahakikishe kwamba wanahifadhi karo ya kuwalipia wanao maana basari hailipi karo yote. Kuna sehemu ambayo mzazi anapasa kulipia.” Alisema.