Kadinali Robert Francis Prevost kutoka Amerika ndiye Papa Mpya

Papa mtakatifu mpya wa kanisa katoliki duniani Leo XIV, Picha/Maktaba
Na Emmanuel Wakoli,
Kadinali Robert Prevost kutoka Amerika, mwenye umri wa miaka 69 alichaguliwa kumrithi Papa Francis aliyefariki dunia Jumatatu ya Pasaka mwaka huu akiwa na umri wa miaka 88 na kuzikwa siku saba baadaye.
Moshi mweupe ulitoka kwenye paa la Kanisa la Sistine Chapel Vatican jijini Roma Alhamisi jioni kutangaza kuchaguliwa kwa kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki lililo na wafuasi zaidi ya 1.4 bilioni kote duniani.
Alichagua jina la Papa Leo XIV na kuwa kiongozi wa 267 wa Wakatoliki duniani.
Umati katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, Vatican ulilipuka kwa shangwe huku kengele zikilia kutoka kwenye kanisa kuu la Vatican, kuthibitisha kwamba makadinali 133 waliokuwa wakishiriki uchaguzi tangu Jumatano walikuwa wamefikia uamuzi wa theluthi mbili kuhusu mrithi wa Papa Francis.
Kufikia mwisho wa duru ya tatu Alhamisi mchana, hakuna aliyekuwa amepata theluthi mbili ya kura za makadinali, hivyo moshi ulikuwa mweusi.
Moshi mweusi wa kikao cha upigaji kura asubuhi ulionekana saa sita na dakika hamsini mchana saa za Kenya, kisha makadinali walichukua mapumziko ya chakula cha mchana.
Hii ilikuwa mara ya pili kuonekana kwa moshi mweusi, baada ya ule wa kwanza kuonekana Jumatano usiku. Hii ilimaanisha kuwa katika duru tatu za mwanzo, hakuna aliyekuwa amewashawishi makadinali 133 wapige kura kumchagua.
Hakuna papa aliyewahi kuchaguliwa katika duru ya kwanza, hivyo moshi mweusi wa Jumatano haukushangaza. Papa Francis, papa wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini, alichaguliwa jioni ya siku ya pili ya mkutano wa uchaguzi mwaka 2013, kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, Benedic XVI, mwaka 2005.
Na ndivyo ilivyokuwa kwa papa mpya Leo XIV. Ulimwengu ulipokuwa ukisubiri ishara ya moshi mweupe, shirika la Reuters liliripoti kwamba alikuwa mmoja wa makadinali tisa waliokuwa “wakitajwa” kuongoza uchaguzini.
Kadinali Robert Prevost ametumia muda mwingi wa maisha yake kama mmishonari Peru na hajulikani sana kimataifa. Alitokea Chicago na amewavutia makadinali wenzake kwa mtindo wake wa kimya.
“Mapapa 10 wa hivi karibuni walichaguliwa wakiwa na wastani wa umri wa miaka 67. Mapapa wawili wa mwisho, Benedict XVI na Francis walikuwa na umri mkubwa kwa viwango vya karne ya 20 walipoanza upapa wao,” iliripoti CNN.