KACHAPIN: NITAHAKIKISHA VIWANDA VYOTE VINAVYOJENGWA KAUNTI HII VINAFUNGULIWA MWAKA HUU.
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi simon Kachapin amewahakikishia wakazi wa kaunti hii kwamba atahakikisha viwanda vyote ambavyo vinajengwa ikiwemo kile cha saruji eneo la Sebit pamoja na cha bidhaa za ngozi cha Nasukuta vinakamilishwa haraka iwezekanavyo.
Akielezea matumaini ya viwanda hivyo kuanza kuhudumu mwaka huu, Kachapin alisema kwamba nia yake kuu hasa katika awamu hii ya pili kama gavana wa kaunti hii ni kuhakikisha kwamba wakazi wananufaika pakubwa na raslimali zilizo kwenye kaunti hii ikiwemo kubuni nafasi za ajira kwa wananchi.
“Kiwanda ambacho kinatengezwa hapo Sebit kitafunguliwa rasmi mwaka huu, na hata kile cha ngozi cha Nasukuta, ili kuhakikisha kwamba wananchi wananufaika na raslimali ambazo zinapatikana katika kaunti hii.” Alisema Kachapin.
Aidha Kachapin aliwataka waakilishi wadi kuharakisha kupasishwa miswada mbali mbali ambayo itapelekea kurahisisha maendeleo katika kaunti hii, akiahidi kwamba serikali yake itashirikiana kwa ukamilifu na viongozi hao kwa manufaa ya wananchi.
“Nashukuru waakilishi wadi wetu kaunti hii. Umoja ambao uko kwa sasa na serikali yangu utapeleka kaunti yetu mbali. Kwa umoja huo wapitishe sheria katika bunge la kaunti ambazo zitapelekea kuhakikisha kwamba kaunti yetu inasonga mbele.” Alisema.
Wakati uo huo Kachapin alisema kwamba serikali yake itahakikisha fedha zinafika kwa wakati katika wadi zote ili kurahisisha juhudi za kuafikia maendeleo kwa wakazi wa maeneo yote ya kaunti hii kwa usawa.
“Ukiona kazi inafanyika, ni gavana ameamua pesa zigatuliwe, zifike mashinani kila wadi ipate maendeleo kwa usawa. Kwa sasa nimepeana milioni 30 kwa kila wadi. Hata basari nimetoa kwa kila mtoto, barabara pia zinaendelea kila sehemu.” Alisema.