KACHAPIN ATEULIWA TENA GAVANA WA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI.


Mwaniaji ugavana katika kaunti hii ya Pokot magharibi kupitia chama cha UDA Simon Kachapin hatimaye ametangazwa mshindi katika kinyang’anyiro cha ugavana kaunti hii.
Hii ni baada yake Kachapin kuibuka mshindi kwenye uchaguzi ambao uliandaliwa jumanne juma hili baada ya kuzoa jumla ya kura alfu 86,476 na kumpiku minzani wake wa Karibu gavana anayeondoka John Lonyangapuo ambaye alipata kura alfu 84,620.
Akizungumza baada ya kutangazwa rasmi kuwa mshindi, Kachapin amewapongeza wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi kwa kumchagua tena kama gavana ili kuendeleza miradi aliyoanzisha katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi kaunti hii.
Aidha kachapin amewapongeza wapinzani wake akiwemo gavana anayeondoka pamoja na naibu gavana Nicholas Atudonyang ambaye pia aliwania kiti hicho kupitia chama cha Kanu.
Akikubali kushindwa gavana John Lonyangapuo amempongeza Kachapin kwa ushindi huo huku akimtaka kuhakikisha kuwa anawahudumia wakazi wote kwa usawa bila ya ubaguzi huku pia akiwataka wakazi wote kudumisha heshima kwa uongozi uliopo licha ya utofauti wa vyama.
Kwa upande wake aliyekuwa mwaniaji wa kiti hicho kwa tiketi ya chama cha KANU Nicholas Atudonyang amempongeza Kachapin kwa ushindi huo, akitumia fursa hiyo pia kumpongeza gavana John Lonyangapuo kwa yale ambayo ameafikia katika kipindi chake akimtaka Kachapin kuendeleza hayo.
Katika wadhifa wa useneta Julius Murgor aliibuka mshindi kwa kupata kura alfu 72,278 huku Geofrey Lipale akiibuka wa pili kwa kura alfu 57,901.
Seneta anayeondoka Samwel Poghisio alikuwa wa tatu kwa kupata kura alfu 41,119.
Katika kinyang’anyiro cha mwakilishi kina mama Rael Kasiwai akiibuka mshindi kwa wadhifa wa mwakilishi kina mama kwa kuzoa kura alfu 67,401.
Mwakilishi kina mama anayeondoka Lilian Tomitom aliibuka wa pili kwa kupata kura alfu 54,122 huku aliyekuwa spika wa bunge la kaunti Catherine mukenyang akiridhia nafasi ya tatu kwa kujizolea kura alfu 43.