KACHAPIN ATETEA UTENDAKAZI WAKE MWAKA MMOJA TANGU ALIPOINGIA AFISINI.

Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameendelea kutetea utendakazi wake mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuongoza kaunti hiyo kwa mara ya pili, huku akiwasuta wakosoaji wake kuwa wanaondeleza siasa zisizo na umuhimu wowote kwa mwananchi wa kaunti hiyo.

Akizungumza na wanahabari Kachapin alisema kwamba katika siku za kwanza 100 baada ya kuingia afisini tayari, alikuwa ametimiza ahadi aliyotoa kwa wakazi wa kaunti hiyo kuhusu swala la mipangilio ya miji na kutoa nafasi kwa wanaomiliki ploti kwenye miji kupata hati miliki.

Aidha Kachapin alisema kwamba japo shughuli hiyo ingali inaendelea kwenye baadhi ya miji katika kaunti hiyo ya Pokot magharibi, anajivunia kwamba angalau hatekelezi shughuli zake nje ya ahadi ambazo alitoa kwa wananchi ikizingatiwa tayari katika baadhi ya miji shughuli hiyo imekamilika.

“Ahadi ambayo nilitoa kwamba katika siku za kwanza 100 nitakuwa nimepangilia maeneo ya miji ili kuwawezesha wanaomiliki ploti kwenye miji kupata hati miliki nilitimiza katika siku hizo 100. Wamiliki wa ploti katika maeneo mengi ya miji kaunti hii sasa wana hati miliki, japo bado shughuli hiyo inaendelezwa katika miji mingine.” Alisema Kachapin.

Wakati uo huo Kachapin alipuuzilia mbali madai kwamba maswala mengi ambayo ametekeleza kufikia sasa ni yale ambayo yalikuwa yameanzishwa na serikali iliyotangulia, akiyataja madai hayo kuwa porojo za kisiasa kwani serikali yake inatekeleza miradi kulingana na manifesto yake.

“Mimi ninafanya kazi kulingana na manifesto yangu. Yapo mambo mengi ambayo nimetekeleza tangu nilipoingia afisini, na wale wanaoeneza madai kwamba nimetekeleza tu yale ambayo yalianzishwa na serikali iliyoondoka ni porojo tu za kisiasa ambazo hazitamsaidia mwananchi wa kaunti hii.” Alisema.