KACHAPIN ASUTA UONGOZI WA LONYANGAPUO KWA KUTEKELEKEZA MIRADI ALIYOANZISHA KATIKA AWAMU YAKE YA KWANZA.

Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameendelea kusuta uongozi wa aliyekuwa gavana John Lonyangapuo kwa kile amesema kutekeleza miradi ambayo alianzisha katika awamu yake ya kwanza ya uongozi.

Akizungumza alipozuru mradi wa ujenzi wa hoteli ya kitalii eneo la Kopoch, gavana Kachapin alisema kwamba hoteli hiyo ni moja ya miradi ambayo ilikusudiwa kufungua kaunti hii hasa kiuchumi kwa kuwavutia watalii zaidi, ikizingatiwa sehemu ambako inajengwa, na inasikitisha kwamba utawala uliotangulia uliamua kuitelekeza kwa misingi ya kisiasa.

Kachapin alisema kwamba atahakikisha hoteli hiyo pamoja na miradi mingine mingi aliyoanzisha katika awamu yake ya kwanza inafufuliwa na kukamilishwa ili raslimali zilizowekwa kwenye miradi hiyo zisipotee, akiwataka viongozi kutoelekeza tofauti zao za kisiasa kwa miradi ambayo inafaa kuwanufaisha wananchi.

“Hii hoteli ilikuwa kubwa sana na ingeleta raslimali nyingi sana kaunti hii iwapo ingekamilishwa. Lengo langu lilikuwa kuwavutia watalii hasa ikizingatiwa eneo ambako niliijenga. Lakini sasa nimekuja kuikamilisha. Nawambia viongozi waache kuingiza tofauti za kisiasa kwa maswala ya maendeleo.” Alisema Kachapin.

Ni kauli ambayo ilisisitizwa na naibu gavana Robert Komole ambaye alisema kwamba kaunti hiyo ingekuwa imeimarika pakubwa kiuchumi kufuatia miradi hiyo iwapo ingekamilishwa na uongozi uliotangulia kwani ingeimarisha pakubwa shughuli za kibiashara.

“Huu mradi ungekamilika ungeimarisha sana biashara eneo hili na hata kusaidia kituo cha kibiashara cha kopoch kuimarika kwa sababu ingewavutia watalii pamoja na wawekezaji wengi, huku wakazi wa eneo hili wakinufaika.” Alisema Komole.