KACHAPIN ASISITIZA HAKIKISHO LAKE LA SHUGHULI ZA MASOMO KUREJELEWA KATIKA SHULE ZILIZOFUNGWA KUFUATIA UTOVU WA USALAMA.

Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameendelea kuwahakikishia wakazi wa maeneo ya mipakani pa kaunti hiyo na kaunti jirani ambako masomo yalitatizika kufuatia utovu wa usalama kwamba shughuli za masomo zitarejelewa kikamilifu mwezi januari  mwaka ujao.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya jamhuri hapo jumanne, Kachapin alisema kwamba hatua ya serikali kuwaajiri maafisa wa usalama wa akiba NPR itasaidia pakubwa katika kuhakikisha kwamba usalama unadumishwa katika shule za maeneo hayo.

“Ile mikakati ambayo tumeweka, nina imani kwamba tutaweza kurejelea shughuli za masomo maeneo ambayo yaliathirika na utovu wa usalama. Na ninaihimiza tume ya huduma kwa walimu TSC kuhakikisha kwamba kuna walimu wakuu wazuri katika shule hizo ambao watafanikisha shughuli za elimu.” Alisema Kachapin.

Kauli yake ilikaririwa na naibu gavana Robert Komole ambaye alisema mikakati ambayo imewekwa na gavana Kachapin inatosha kuhakikisha shughuli za masomo zinarejelewa, ili watoto wa maeneo hayo pia wapate haki sawa kwa elimu kama wenzao maeneo mengine ya nchi.

“Tunashukuru kwa mikakati ambayo imewekwa kuhakikisha kwamba shule ambazo zilifungwa maeneo ya mipakani pa kaunti hii zinafunguliwa tena, na kuwapa fursa wanafunzi wa eneo hilo kupata elimu kama watoto maeneo mengine ya nchi.” Alisema Komole.

Kwa upande wake kamishina wa kaunti hiyo Apolo Okelo alitoa wito kwa viongozi katika kaunti hiyo kushirikiana na idara ya usalama ili kuhakikisha kwamba maeneo machache ambayo yanakabiliwa na utovu wa usalama kaunti hiyo yanapata usalama.

“Tuna maeneo machache tu ambayo bado tunashuhudia utovu wa usalama hasa kule Chesogon na Sarmach. Nawahimiza viongozi wote kushirikiana na idara za usalama kuhakikisha kwamba tunaafikia amani maeneo hayo.” Alisema Apolo.