KACHAPIN ASHINIKIZA SHULE ZILIZOFUNGWA KUTOKANA NA UTOVU WA USALAMA KUFUNGULIWA JANUARI.

Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ametoa wito kwa serikali kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba masomo yanarejelewa mwezi januari, katika shule ambazo zilifungwa maeneo ambayo yamekuwa yakishuhudia utovu wa usalama katika kaunti hiyo.

Kachapin alisema kwamba yeye kama gavana wa kaunti hiyo amefanya kila juhudi ikiwemo kuandaa mazungumzo na wakazi wa maeneo hayo katika juhudi za kuhakikisha kuna amani, na sasa ni jukumu la idara husika kuhakikisha kwamba hali ya usalama inadumishwa maeneo hayo.

Akizungumza katika hafla ya kuchangisha fedha kwenye kanisa la ACK Talau, Kachapin aidha aliitaka wizara ya elimu kwa ushirikiano na baraza la mitihani nchini KNEC, kuhakikisha kwamba watahiniwa ambao walikosa kufanya mitihani ya kitaifa kufuatia utovu wa usalama kaunti hiyo wanafanya mitihani hiyo.

Zile shule ambazo ziliathiriwa na utovu wa usalama zifunguliwe januari bila kukosa. Haitakuwa vyema shule zikirejelea shughuli za masomo januari huku hizi zikisalia kufungwa. Pia kuna shule ambazo hazikufanya mtihani wa kitaifa. Wale wanaohusika ni lazima wazingatie hilo kwa sababu ni jukumu lao.” Alisema Kachapin.

Ni kauli ambayo ilikaririwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto, akitaja mipaka kati ya kaunti hiyo na kaunti jirani za Turkana na Elgeyo Marakwet kuwa sugu katika visa hivyo, akielezea haja ya wakuu wa usalama kuandaa kikao na wazee katika kaunti hizi ili kupata suluhu ya kudumu kwa tatizo hili la miaka mingi.

“Hili swala la utovu wa usalama bado linashuhudiwa hasa maeneo ya mipaka ya kaunti hii na kaunti za Turkana na Elgeyo Marakwet. Na ombi letu ni kwamba serikali iingilie, izungumze na wazee ili kutafuta mbinu ya kumaliza tatizo hili ambalo limedumu kwa miaka mingi.”Alisema Moroto.