KACHAPIN APUUZILIA MBALI MADAI YA KUWAFUTA KAZI WAFANYIKAZI WA KAUNTI WALIOAJIRIWA NA JOHN LONYANGAPUO.
Gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Kachapin amepinga vikali madai kwamba amewafuta kazi wafanyikazi wa umma waliokuwa wakihudumu katika serikali ya aliyekuwa gavana John Lonyangapuo punde alipoingia uongozini.
Katika mahojiano na wanahabari Kachapin alisema kwamba waliositisha huduma zao serikalini walifanya hivyo baada ya kukamilika kandarasi walizosaini kuhudumu.
Alisema kwamba wafanyikazi wa kaunti hutia saini kandarasi mpya kila baada ya kukamilika miezi mitatu ya kuhudumu, na muda wa kuhudumu unapokamilika hawana budi kusitisha huduma zao akisisitiza hamna mfanyikazi yeyote aliyefutwa kazi.
“Sijamfuta kazi mtu yeyote mimi. Wafanyikazi wa kaunti hufanya kazi kwa kandarasi ya miezi mitatu na inapokamilika wanasaini kandarasi nyingine au kubadilishwa. Kwa hivyo wale ambao waliondoka walifanya hivyo kwa sababu kandarasi yao waliotia sahihi ilikamilika.” Alisema Kachapin.
Wakati uo huo Kachapin alisema kaunti ya Pokot magharibi ilikuwa na wafanyikazi hewa wengi na hivyo alilazimika kufanyia ukaguzi wafanyikazi wanaolipwa na serikali na kuwaondoa wale ambao wanalipwa bila kutoa huduma zozote serikalini.
“Kaunti hii iliorodheshwa na baadhi ya magazeti nchini kuwa miongoni mwa kaunti ambazo zilikuwa na wafanyikazi hewa wengi. Watu walikuwa wanapata mishahara na hawafanyi kazi. Kwa hivyo watu kama hawa tuliwaondoa na ndipo unaona watu wakisema nimewafuta kazi.” Alisema.