KACHAPIN AMSUTA LONGAPUO KWA KUHUJUMU MIRADI ALIYOANZISHA POKOT MAGHARIBI.


Mgombea ugavana katika kaunti hii ya Pokot magharibi kwa tiketi ya chama cha UDA Simon Kachapin ameendelea kuelezea sababu za kutaka kupewa fursa nyingine kuongoza kaunti hii katika uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti mwaka huu.
Kachapin ambaye alikuwa gavana wa kwanza wa kaunti hii ya Pokot magharibi amesuta utawala wa gavana wa sasa John Lonyangapuo akisema kuwa amevuruga msingi wa maendeleo alioweka wakati akihudumu kama gavana wa kwanza wa kaunti hii.
Kachapin amedai utawala wa gavana Lonyangapuo umefeli kutokana na hali kuwa amekuwa akiwateua maafisa kuhudumu katika idara ambazo hawana ujuzi na ufahamu kuzihusu.
Kachapin amesema kuwa atashirikiana kikamilifu na serikali kuu ili kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inafanikishwa kaunti hii na kuimarisha maisha ya wakenya iwapo atapewa fursa ya kuongoza tena kaunti hii baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi agosti.