KACHAPIN AENDELEZA MIKAKATI YA KUIMARISHA SEKTA YA AFYA POKOT MAGHARIBI.

Gavana wa kaunti hii ya Poko magharibi Simon Kachapin aliandaa jana jioni kikao na balozi wa Denmark humu nchini Ole Thonke katika makao makuu ya ubalozi wa taifa hilo ulioko eneo la Gigiri jijini Nairobi.

Mazungumzo baina ya wawili hao yalijikita katika ushirikiano kwenye sekta ya afya, juhudi za kuafikia amani na usalama katika kanda hii.

Gavana Kachapin aliupongeza ubalozi huo wa Denmark kufuatia juhudi zake kuliunga mkono taifa la Kenya hasa katika sekta ya afya akisisitiza haja ya kuimarisha zaidi ushirikiano huo kwa lengo la kuafikia matokeo bora katika sekta ya afya nchini.

Aidha katika kikao hicho iliafikiwa kuwa ubalozi huo utafanya kazi na serikali ya kaunti hii kuimarisha usalama kwenye mipaka ya kaunti hii na kaunti jirani za Baringo na Turkana.

Ikumbukwe mwezi uliopita Kachapin alitangaza mabadiliko makubwa katika sekta ya afya ili kuimarisha huduma, Kachapin akisema kwamba ushirikiano huu na baadhi ya washirika unadhihirisha kujitolea kwa serikali yake kuimarisha sekta ya afya na kuafikia malengo ya huduma za afya kwa wote.