‘JUKUMU LA KUJILINDA DHIDI YA CORONA NI LA MWANANCHI MWENYEWE’ ASEMA POGHISIO.


Seneta wa kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ameendelea kusisitiza haja ya wakazi wa kaunti hii kuwa makini zaidi dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona msimu huu ambapo watu wanakusanyika kwa sherehe mbali mbali ikiwemo ile ya kuvuka mwaka.
Akizungumza katika mahojiano na kituo hiki Poghisio amesema kuwa ni jukumu la mwananchi mwenyewe kujilinda dhidi ya maambukizi haya hasa ikizingatiwa kile ametaja kuwa huduma duni katika sekta ya afya kutokana na ukosefu wa vifaa vya kuwahudumia wagonjwa katika hospitali za kaunti hii.
Poghisio ametumia fursa hiyo kuishutumu serikali ya kaunti hii kwa kile amedai imefuja fedha ambazo zilinuiwa kutumika kuimarisha sekta ya afya huku hospitali na vituo mbali mbali vya afya vikisalia bila huduma zinazostahili kwa mwananchi.
Wakati uo huo Poghisio ambaye pia ni kiongozi wa wengi katika bunge la seneti ametaka wakazi ambao hawajapokea chanjo dhidi ya virusi vya corona kutumia fursa hii kupokea chanjo hiyo ambayo inaendelea kutolewa katika vituo mbali mbali vya afya ili kusalia salama dhidi ya janga la corona.