JUHUDI ZAIDI ZAHITAJIKA KUKABILI MIMBA ZA MAPEMA POKOT MAGHARIBI.

NA BENSON ASWANI
Licha ya visa vya mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi wa kike kuonekana kushuka katika kaunti hii ya Pokot magharibi, ipo haja ya wadau kutia juhudi katika kubuni mikakati ya kuhakikisha kuwa visa hivi vinakabiliwa vilivyo ili kumpa mtoto wa kike fursa ya kutimiza ndoto zake maishani.
Kulingana na mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya Propoi kaunti hii Jamas Murray takwimu zilizochukuliwa mwaka jana ziliashiria wazi kuwa visa hivi bado vinaripotiwa kwa viwango vya kutia wasiwasi na kuwa jamii inafaa kuimarisha vita dhidi ya visa hivi.
Aidha Murray amesema kuwa kinyume na dhana kuwa vingi vya visa hivi husababishwa na watu wazima, wahusika wakuu ni vijana wadogo na kuwa imekuwa vigumu kukabiliana navyo kutokanba na hali kuwa jamii za wahusika hukubaliana kusuluhisha swala hilo nje ya mahakama.
Wakati uo huo Murray ameelezea wasi wasi kuwa huenda visa zaidi vya mimba za mapema vikashuhudiwa ikizingatiwa likizo ndefu ambayo wanafunzi wanatarajiwa kusalia nyumbani kuanzia mwezi machi wakati wa mitihani ya kitaifa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha nne na darasa la nane.