Jopo la kuangazia dhuluma za jinsia laandaa vikao vya umma

Wakaazi wa kaunti ya pokot magharibi wakitoa maoni kuhusu dhuluma za kijinsia, Picha/Benson Aswani
Na Benson Aswani,
Jopokazi la kuangazia swala la dhuluma za jinsia linaendeleza zoezi la kuwahusisha wananchi katika kaunti ya Pokot magharibi katika moja ya mikakati ya serikali ya kitaifa kukabili dhuluma hizi miongoni mwa jamii.
Kulingana na wanachama wa jopo hilo wakiongozwa na Harleen Kaur Jabbal, wanalenga kupata maoni kutoka kwa wakazi hasa maeneo ya mashinani ambao wamepitia dhuluma hizi ikiwemo ukeketaji, ndoa za mapema miongoni mwa maswala mengine ambayo yanapelekea dhuluma za jinsia ili kupata suluhu kwa uovu huo.
“Tunatazamia kupata maoni kutoka kwa wanachi hasa maeneo ya mashinani, tukiwalenga hasa waathiriwa wa visa hivi vya dhuluma za kijinsia, ili tumsaidie rais katika vita dhidi ya uovu huu,” alisema Bi. Harleen
Naibu gavana kaunti hiyo Robert Komole alipongeza mwelekeo huo katika vita dhidi ya dhuluma za jinsia anazosema zinasababishwa pakubwa na umasikini na ukosefu wa elimu, akiahidi ushirikiano mkamilifu wa serikali ya kaunti kuhakikisha jopo hilo linaafikia malengo yake.
“Nakubali kwamba ni muhimu kupata maoni kutoka kwa wananchi kuhusu swala hili la dhuluma za jinsia. Na kama kaunti tunaahidi kushirikiana na jopo hili katika shughuli hii nzima ili kuhakikisha kwamba linaafikia malengo yake,” alisema Komole.
Kwa upande wake kamishina wa kaunti hiyo ya Pokot magharibi Abdulahi Khalif alisema vita hivi vimelemazwa kutokana na wahusika kutoripoti kwa idara husika na badala yake kuamua kuvisuluhisha nyumbani.
“Matukio ya watu kusuluhisha visa hivi nyumbani yameenea sana katika kaunti hii. Tunawachunguza baadhi ya maafisa wetu wakiwemo machifu na maafisa wa usalama ambao wanahusika katika kusuluhisha kesi hizi nyumbani,” alisema Bw. Khalif.