JOPO LA KUANGAZIA CBC LAZURU POKOT MAGHARIBI HUKU MTAALA HUO UKIENDELEA KUPOKEA PINGAMIZI


Baadhi ya wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi wameendelea kupinga utekelezwaji wa mtaala mpya wa elimu CBC huku jopo lililobuniwa na rais William Ruto likiendeleza vikao vya mwisho mwisho kukusanya maoni kuhusu utekelezwaji wa mtaala huo.
Wakizungumza baada ya vikao vya jumatano na jopo hilo, baadhi ya wakazi walisema kuwa utekelezwaji wa mtaala huo unapasa kuahirishwa kwani taifa halikuwa tayari kuutekeleza huku baadhi wakitaka uondolewe kabisa wakidai una gharama ya juu kwa mzazi.
“Sipendi CBC kwa sababu ya gharama yake ya juu. Kwa sasa maisha yamekuwa magumu na watu wengi hawajiwezi kimaisha. Kwa sasa wengi wetu tunafikiria kuhusu jinisi ya kupata chakula si tena kugharamika kununua vitu shuleni kwa sababu ya CBC.” Walisema wakazi.
Gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Kachapin alisema kwamba mtaala wa CBC ni bora zaidi ila utekelezwaji wake ndio uliharakishwa hata kabla ya wadau husika ambao ni walimu kujiandaa kikamilifu kuutekeleza, akipendekeza marekebisho kadhaa katika utekelezwaji wake.
“Mtaala wa CBC ni mzuri lakini utekelezwaji wake uliharakishwa. Ilifaa kuhusishwa wadau wote hasa walimu ili kuwapa nafasi ya kuulewa vyema kabla ya kutekelezwa rasmi nchini. Hata hivyo unaweza kufanyiwa marekebisho ili kuwafaa wahusika wote.” Alisema Kachapin.
Kwa upande wake mwanachama wa jopo hilo aliyeongoza vikao hivyo katika kaunti hii Prof. David Some alisema kwamba vikao hivyo vitakamilishwa siku ya ijumaa kote nchini kabla ya maoni yote kujumishwa na kuandaa ripoti itakayowasilishwa kwa rais William Ruto.
“Kufikia mwisho wa ijumaa tutakuwa tumezuru kaunti zote nchini kwani tuko vikundi kumi katika mchakato huu. Tutayaweka pamoja maoni ya wakenya kutoka maeneo mbali mbali ya nchi kuhusu mtaala huu na kisha kuandaa ripoti ambayo tutamkabidhi rais.” Alisema Some.